Rais Samia Suluhu Hassan, amekutana na Wagombea wa urais na wagombea wenza kutoka vyama vya siasa 16 vilivyo shiriki katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 na kujadili kuhusu namna ya kuimarisha maridhiano ya kisiasa, demokrasia ya vyama, amani na mshikamano wa kitaifa.
Hatua hiyo, imekuja miezi mitano tangu uchaguzi huo ufanyike na kumpata Rais Samia aliyegombea kwa tiketi ya CCM ushindi wa zaidi ya asilimia 96 na baadaye akaapishwa kuiongoza Tanzania kwa muhula wa pili.
Katika uchaguzi huo, Samia alishindana na wagombea 16 kutoka vyama mbalimbali vya siasa, ambao wote ndio waliohudhuria kikao hicho na mkuu huyo wa nchi kujadili kuhusu mustakabali wa Taifa.

Taarifa ya kikao hicho, imetolewa leo, Jumatano Aprili 1, 2026 na kutiwa saini na Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Shaaban Kissu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wanasiasa hao, walitumia nafasi hiyo kuwasilisha maoni yao kuhusu namna ya kuimarisha maridhiano ya kisiasa, demokrasia ya vyama, amani na mshikamano wa kitaifa baada ya uchaguzi mkuu.

Pia, wametoa maoni kuhusu namna ya kuimarisha ushiriki wa wananchi katika shughuli za maendeleo na kudumisha tunu za umoja wa kitaifa.
