Masoko ya kimataifa yamepumua kwa afueni baada ya bei ya mafuta kushuka kwa kasi na hisa kupanda, kufuatia tangazo la kusitishwa kwa mapigano kwa masharti kati ya Marekani na Iran lililotolewa na Rais wa Marekani, Donald Trump.
Katika hatua iliyokuja saa chache kabla ya muda wa mwisho wa mashambulizi ya kijeshi, Trump amekubali kuahirisha tishio lake la kuishambulia Iran, kwa masharti kwamba Tehran ikubali kusitisha mapigano kwa muda wa wiki mbili na kufungua njia muhimu ya usafirishaji wa mafuta duniani, ya mlango wa bahari wa Hormuz.
Athari za tangazo hilo zilionekana haraka katika masoko ya nishati, ambapo bei ya mafuta ghafi aina ya Brent, kipimo cha kimataifa, ilishuka kwa karibu asilimia 15 hadi kufikia dola 93 (Sh239,307) kutoka dola 114 (Sh293,346) kwa pipa.
Hatua hiyo ilifuatia ahadi ya Iran kuruhusu tena usafirishaji wa mafuta kupitia mlango wa Hormuz chini ya usimamizi wa jeshi lake.
Wakati huohuo, mafuta ghafi ya Marekani pia yalishuka kwa kiwango kikubwa, ishara kwamba wawekezaji walikuwa wakitarajia kurejea kwa mtiririko wa mafuta katika soko la dunia baada ya wiki kadhaa za taharuki.
