Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Prof. Riziki Shemdoe, amezielekeza Halmashauri nane nchini kutumia kwa uaminifu shilingi bilioni 5.2 zilizotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Mitaji (UNCDF) kupitia mradi wa LoCAL.
Fedha hizo zilizokabidhiwa jijini Dodoma, zimeelekezwa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi ili kuwaletea wananchi maendeleo yaliyokusudiwa.
Prof. Shemdoe amebainisha kuwa utekelezaji mzuri wa awamu ya kwanza katika wilaya za Chamwino, Kondoa, na Mpwapwa umefungua milango ya kupatikana kwa mradi mpya wa SCALE utakaonufaisha halmashauri 54 nchini.
Amesisitiza kuwa diplomasia ya uchumi ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ndiyo inayovutia wadau wa maendeleo, na kutoa wito kwa wadau wengine zaidi kujitokeza kushirikiana na Serikali.
Kufuatia maelekezo hayo, waratibu na maafisa mazingira kutoka Halmashauri za Kondoa, Chamwino, na Mpwapwa wamethibitisha kupokea mgawo wao wa fedha hizo.
Wameeleza kuwa zitatumika kutekeleza awamu ya pili ya mradi huo kupitia kilimo cha kisasa, uchimbaji wa visima vya umwagiliaji, na ujenzi wa mifereji ili kuimarisha usalama wa chakula kwa wananchi.
