Nguli wa muziki kutoka Mali, Salif Keita, ameshindwa kupanda jukwaani katika Tamasha la Sauti za Busara 2026 kutokana na matatizo ya kiafya.
Msanii huyo mkongwe alitarajiwa kuwa ndiye atakayefunga tamasha hilo Februari 8, 2026, lakini hali yake ya kiafya ilimlazimu kukosa safari na kushindwa kushiriki tukio hilo muhimu la muziki barani Afrika.
Akizungumza kuhusu kutokuwepo kwa Salif Keita, Mkurugenzi wa Tamasha la Sauti za Busara, Journey Ramadhan, amesema licha ya changamoto hiyo, tamasha limefanyika kwa mafanikio makubwa.
Ameeleza kuwa taarifa rasmi kutoka kwa madaktari wa msanii huyo ilielekeza kuwa hakuwa katika hali ya kuruhusiwa kusafiri na kushiriki tamasha hilo.
Katika hatua nyingine, Journey ametangaza kuwa tamasha la Sauti za Busara 2027, ambalo litakuwa msimu wa 24, litafanyika mwezi Machi badala ya Februari kama ilivyozoeleka kwa miaka ya nyuma.
