Na Michael Mpunije- Kasulu, Kigoma
KASULU: Maafisa Usafirishaji maarufu bodaboda wilayani Kasulu Mkoani Kigoma wametakiwa kuepuka kuwa chanzo cha vitendo vya uhalifu na uvunjifu wa amani badala yake washirikiane na vyombo vya ulinzi na usalama kufichua wahalifu.
Wito huo umetolewa leo Februari 10, 2026 na Mratibu wa Polisi Jamii wilaya ya Kasulu, Mkaguzi msaidizi wa Polisi Inspector Willy Lupa wakati akizungumza na maafisa usafirishaji wilayani humo na kueleza umuhimu wa bodaboda kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama.

Amesema baadhi ya maafisa usafirishaji hao wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya uhalifu ikiwemo kukwapua mikoba na simu jambo ambalo linaendelea kuharibu taswira na sifa za bodaboda huku akitia wito wa kuhakikisha wanashirikiana kuimarisha ulinzi shirikishi ikiwemo kutoa taarifa za viashiria vya uvunjifu wa Amani.
Kwa upande wao baadhi ya maafisa usafirishaji maarufu bodaboda wilaya ya Kasulu wamesema kupitia vikundi vyao wameweka nakutekeleza sheria mbalimbali ikiwemo kuchukua hatua kwa baadhi ya wale wanaobainika wakijihusisha na vitendo vya uhalifu kwa lengo la kudumisha amani katika jamii ikiwa ni pamoja na kulinda heshima na sifa za kazi hiyo.
