Baraza la Maaskofu Katoliki la Sudan na Sudan Kusini limetoa wito wa kufanyika kwa uchaguzi huru, wa haki na wa kuaminika nchini Sudan Kusini, kusitishwa mara moja kwa mapigano nchini Sudan, pamoja na hatua za haraka za kukabiliana na changamoto za kibinadamu zinazowakabili wananchi wa mataifa hayo mawili.
Maaskofu hao wameonya kuwa kuendelea kwa migogoro ya kisiasa, ukosefu wa usalama, vita na uhaba wa chakula kunazidi kudhoofisha utu, maisha na matumaini ya wananchi.
Wito huo umetolewa katika taarifa ya mwisho ya Mkutano Mkuu wa 52 wa Baraza hilo uliofanyika mjini Torit, Sudan Kusini, kuanzia Novemba 7 hadi 13, mwaka 2026.
Katika taarifa hiyo iliyosainiwa na Rais wa Baraza hilo, Kardinali Stephen Ameyu Martin Mulla, ambaye pia ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Juba, Maaskofu wamewataka viongozi wa kisiasa, Jumuiya ya Kimataifa na wananchi kwa ujumla kuweka mbele masuala ya amani, utawala wa kikatiba, uwajibikaji na maendeleo ya wananchi.
Kuhusu hali ya kisiasa nchini Sudan Kusini, Maaskofu wameeleza wasiwasi wao juu ya maandalizi yasiyoridhisha ya uchaguzi mkuu, ambao awali ulipangwa kufanyika Desemba 22, mwaka 2026, lakini sasa unatarajiwa kufanyika Februari 11, mwaka 2027.
Wamesema changamoto zinazohusisha maandalizi ya kitaasisi, kiufundi, kifedha na kiusalama, pamoja na kutokamilika kwa majukumu ya kipindi cha mpito na kutokuaminiana miongoni mwa viongozi wa kisiasa, vinaweza kuathiri uaminifu wa uchaguzi huo.
Hivyo, wameitaka Serikali ya Mpito, Tume ya Taifa ya Uchaguzi na wadau wengine wa kisiasa kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru, shirikishi, wa wazi na wa amani.
Aidha, wametaka mazungumzo ya dhati kati ya Serikali, viongozi wa upinzani na makundi ambayo bado hayajasaini makubaliano ya amani, huku wakisisitiza umuhimu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kufanya kazi kwa uhuru bila kuingiliwa kisiasa.
Maaskofu pia wametaka wanawake, vijana, watu wenye ulemavu, wakimbizi wa ndani na makundi mengine yaliyotengwa kupewa nafasi ya kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi.
Kwa upande wa Sudan, Maaskofu wamekemea vikali vita vinavyoendelea kati ya Jeshi la Sudan, SAF, na Vikosi vya Usaidizi wa Haraka, RSF, wakieleza kuwa mapigano hayo yamesababisha vifo, uharibifu wa nyumba, shule, hospitali na maeneo ya ibada, pamoja na kulazimisha maelfu ya wananchi kuyahama makazi yao.
Wamezitaka pande zinazopigana kusitisha mapigano mara moja, kulinda raia, kuruhusu misaada ya kibinadamu kufikishwa bila vikwazo na kuheshimu sheria za kimataifa za kibinadamu.
Vilevile, wameeleza wasiwasi kuhusu vitisho vinavyokabili jumuiya za Kikristo, mapadre, watawa na taasisi za Kanisa, wakisisitiza kuwa uhuru wa dini na dhamiri ni haki ya msingi ya kila binadamu.
Katika hatua nyingine, Maaskofu wameonya kuhusu kuongezeka kwa uhaba wa chakula na athari za mabadiliko ya tabianchi katika mataifa hayo mawili, wakieleza kuwa wanawake, watoto, wakulima wadogo na familia za vijijini wako katika hatari kubwa ya kukumbwa na njaa.
Wamezitaka Serikali na wadau wa maendeleo kuimarisha misaada ya chakula, kusaidia wakulima kwa mbegu na zana za kilimo, kuboresha mifumo ya umwagiliaji na upatikanaji wa maji, pamoja na kuwekeza katika uzalishaji endelevu wa chakula.
Kuhusu afya ya umma, Maaskofu wameonesha wasiwasi juu ya hatari ya kuenea kwa ugonjwa wa Ebola na magonjwa mengine ya kuambukiza, hasa katika maeneo yanayopakana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Wametaka kuimarishwa kwa mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa, huduma za afya, elimu kwa wananchi na ushirikiano wa kukabiliana na magonjwa katika maeneo ya mipakani.
Aidha, wamezitaka Serikali na jamii kuwekeza zaidi kwa vijana kupitia elimu bora, mafunzo ya ufundi stadi, ajira na ujasiriamali, huku wakiwataka vijana kukataa vurugu, chuki, matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii na kutumiwa kwa maslahi ya kisiasa.
Wakisisitiza nafasi ya Kanisa katika ujenzi wa amani, Maaskofu wamesema Kanisa Katoliki litaendelea kutoa huduma za kiroho, elimu, afya, misaada ya kibinadamu, upatanisho na utetezi wa haki za binadamu bila kuunga mkono chama chochote cha kisiasa au mgombea.
Wakirejea mafundisho ya Papa Francisko katika Waraka wa Kitume Fratelli Tutti, wameeleza kuwa siasa zinazolenga manufaa ya wote ni wito wa huduma na upendo kwa jamii, hivyo uongozi haupaswi kutumika kwa manufaa binafsi.
Katika kuhitimisha taarifa yao, Maaskofu wamewataka viongozi kuchagua mazungumzo badala ya migawanyiko, haki badala ya kisasi na huduma badala ya maslahi binafsi.
Pia wamewaalika mapadre, watawa na waamini kuendelea kuliombea taifa la Sudan na Sudan Kusini, ili Mungu ayajalie mataifa hayo amani, haki, umoja na maendeleo endelevu.
Maaskofu hao wamehitimisha kwa kusisitiza kuwa wananchi wa Sudan na Sudan Kusini wameteseka vya kutosha na kwamba wakati umefika wa matumaini yao kuonekana katika matendo ya kweli ya amani, haki na uwajibikaji.
