DAR ES SALAAM: Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameondoka nchini leo Februari 12, 2026 kuelekea Addis Ababa, Ethiopia kushiriki Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU), utakaofanyika Februari 14 na 15, 2026.
Kabla ya mkutano huo mkuu, Rais Samia anatarajiwa kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (CAHOSCC) utakaofanyika Februari 13, 2026, chini ya uenyekiti wa Rais wa Kenya, William Ruto, na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Afrika.
Akiwa Ethiopia, Rais Samia pia anatarajiwa kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na viongozi kadhaa wa Afrika na taasisi za kikanda, ikiwemo Waziri Mkuu wa Eswatini, Rais wa Comoro, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kisiasa, kiuchumi na maendeleo.
Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Umoja wa Afrika utafanyika sambamba na kutangazwa rasmi kwa uongozi mpya wa Umoja huo kwa mwaka 2026, ambapo Burundi itachukua nafasi ya Uenyekiti, Tanzania itateuliwa kuwa Makamu wa Pili wa Mwenyekiti, huku Kanda ya Mashariki ikipewa nafasi ya Nchi Wanachama katika uongozi wa AU.
Katika mkutano huo, Tanzania pia inakamilisha rasmi kipindi chake cha kuhudumu katika Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika kwa awamu mbili mfululizo kuanzia 2022 hadi 2026, hatua inayothibitisha mchango wa nchi katika kuimarisha amani, usalama na utulivu barani Afrika.

