Na Samwel Masunzu- Kibondo, Kigoma
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma Bw. Diocles Rutema amewaagiza maafisa watendaji wa kata kwa kushirikiana na madiwani, ili kuhakikisha watoto ambao hawajaripoti shuleni watafutwe na ijulikane mahali walipo
Wanafunzi ambao wamefaulu na kupangiwa kuripoti kuanza masomo ya kidato cha kwanza kwa mwaka huu 2026 katika halmashauri ya wilaya Kibondo ni wanafunzi 3450 na ambao hawajaripoti hadi kufikia Februari 11 ni wanafunzi 189 pekee sawa na asilimia 6 tofauti na miaka iliyopita
Mkurugenzi Mtendaji Rutema kupitia kikao cha baraza la madiwani cha kupokea na kujadili taarifa za shughuli zilizofanyika kwa robo ya pili kwa mwaka wa fedha 2025-26 amezipongeza kata ambazo wanafunzi wote wamesharipoti shuleni ambazo ni Misezero, Itaba, Murungu na Kitahana
Rutema amezitaja shule ambazo wanafunzi wake hawajaripoti wafuatiliwe ikiwemo Biturana, Kigina, Muramba na Kisogwe lengo likiwa ni kufikia asilimia 100 ya watoto wote kuripoti shuleni
Mwenyekiti wa Chama cha mapinduzi CCM wilaya ya Kibondo Hamis Tahiro amepongeza jitihada hizo huku mwenyekiti wa chama cha ACT Wazalendo Nicholaus Kilunga akieleza kuwa changamoto ndogondogo zikiwemo za madawati ziendelee kutafutiwa ufumbuzi.
Akifunga kikao hicho mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kibondo ambaye ni diwani wa kata Kibondo mjini Bw. Alex Baragomwa amewataka madiwani kuendeleza ushirikiano ili kutimiza mahitaji ya wananchi.
