Kampuni ya mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML) imebainisha kuwa takribani shilingi bilioni 70 zinatarajiwa kulipwa kama fidia ya wananchi kwa ajili ya kupisha shughuli za mgodi.
Afisa Mahusiano Mwandamizi wa GGML Gilbert Mworia amesema hayo katika kikao maalum cha kutathimini bajeti cha kamati ya ushauri mkoa mahususi kwa kujadili utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2025/26.

Mworia amesema kuwa mpango wa malipo ya madai hayo unatamatisha kilio cha miaka 25 cha maombi ya fidia kwa wakazi wa mitaa ya Nyakabale na Nyamalembo iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Geita Mkoani humo.
Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela ameagiza upembuzi yakinifu kufanyika kabla ya kuanza kwa malipo ya fidia kwa wananchi wanaopisha shughuli za GGML ili kuongeza ufanisi wa malipo na haki kutendeka.

Makisio ya pesa hiyo ni kwa mujibu wa tathimini ya awali ya fidia kwa wananchi ambayo imechukua miezi 6 tangu ilipoanza kufanyika rasmi Agosti 21, 2025 na inatarajiwa kukamilika machi 4, 2026 ili wahusika waliopisha maeneo wasaini mikataba yao kwaajiri ya malipo.
