Katibu wa NEC, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi, amepongeza utekelezaji wa miradi ya nishati nchini akisema ni sehemu ya dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kupanua matumizi ya nishati na kukuza uchumi wa Watanzania.
Kihongosi ametoa kauli hiyo baada ya kukagua mradi wa kufua umeme kwa kutumia nishati ya jua uliotekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi kwa gharama ya shilingi bilioni 11 katika Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu.
Amesema miradi hiyo ina mchango mkubwa katika kuimarisha upatikanaji wa umeme na kuchochea shughuli za kiuchumi kwa wananchi.
Kwa upande wake, Meneja wa TANESCO katika Halmashauri ya Ushetu, George Madaha, amesema mradi huo unazalisha megawati tano za umeme zinazounganishwa kwenye gridi ya taifa na umewezesha wananchi takribani 11,000 kunufaika na huduma ya umeme.
Naye Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba, amesema Serikali inaendelea kupeleka umeme katika vitongoji 130 vya Halmashauri ya Ushetu, akibainisha kuwa mpango uliopo ni kuhakikisha hadi kufikia mwaka 2029 vitongoji vyote vya Mkoa wa Shinyanga vinapata huduma ya umeme.
Baadhi ya wananchi wa eneo hilo wamesema mradi huo umeondoa changamoto ya kukatika kwa umeme iliyokuwa ikitokea mara kwa mara, jambo linalosaidia kuimarisha shughuli za kiuchumi na kuboresha maisha yao.
