Shirika la mpango wa chakula duniani (WFP) limeeleza kuridhishwa na utekelezaji wa mradi wa kilimo tija Kigoma KITIKI unaotekelezwa mkoani Kigoma
Mradi huo unatekelezwa katika halmashauri nne za mkoa wa Kigoma ambazo ni Kasulu vijijini , Kasulu Mji, Kibondo na Kakonko ukisimamiwa na shirika la WFP na kutekelezwa na mashirika mengine ambayo ni World Vision Tanzania pamoja na Good neighbors Tanzania
Akiwa kwenye maadhimisho ya siku ya wakulima kwenye kijiji cha Katanga wilayani Kakonko mkoani Kigoma na kukagua shamba darasa la kikundi cha Kwizera, Meneja mradi wa KITIKI kutoka shirika la WFP – Kasulu Bw. Hyoyedl Lee Amesema shirika linaridhishwa na namna ambavyo mradi huo unatekelezwa
Hyoyeld Lee amesema shirika la WFP limekuwa likishirikiana na wadau wengine ikiwemo serikali ya Tanzania, wauzaji wa pembejeo za kilimo,wazalishaji na wasambazaji wa mbegu ili ziweze kuwafikia wakulima
Mwakilishi wa Meneja wa mradi huo kutoka shirika la World Vision Tanzania mkoa wa Kigoma Bw. Samson Katabila amesema shirika limekuwa likitoa elimu kwa wakulima kuhusu namna bora ya kuongeza uzalishaji na kuepuka upotevu wa mazao
Amesema wakulima kupitia mradi wanapata pembejeo za kilimo pamoja na mbegu bora zinazoleta tija kwa wakulima tofauti na mbegu ambazo walikuwa wakizitumia
Mwenyekiti wa kikundi cha wakulima cha Kwizera –Katanga Bw. Yusufu Ngaye ameyashukuru mashirika yanayotekelea mradi huo kwa kuwapatia elimu ya kilimo na pembejeo za kilimo hali ambayo imeongeza uzalishaji tofauti na kilimo kilichozoeleka
Mgeni rasmi katika sherehe hiyo, diwani wa kata ya Katanga Bw. Ezekiel Bikata amewaasa wakulima waliopata elimu kupitia mradi huo, kuendelea kutumia elimu hiyo katika uzalishaji wa mazao na elimu hiyo isiishie kwenye vikundi, bali iwe chachu kwa jamii nzima katika kuongeza wigo wa uzalishaji na kwamba viongozi wataendelea kuhakikisha elimu hiyo inamfikia kila mmoja
Mradi wa kilimo Tija Kigoma KITIKI ulianza mwaka 2023 ukitekelezwa na mashirika ya World Vision Tanzania pamoja na Good neighbors Tanzania yakisimamiwa na shirika la mpango wa chukula duniani WFP kwa ufadhiri kwa serikali ya Korea kusini kupitia shirika lake la maendeleo KOICA lengo likiwa ni kuimarisha uwezo wa wakulima wadogo kwa kuwapatia elimu bora katika kilimo cha mahindi,maharage na alizeti ,mafunzo ambayo yamekuwa yakitolewa kwa nadharia na vitendo na mradi utamalizika mwezi Machi 2027
