Mfanyabiashara na mwekezaji wa Tanzania, Rostam Aziz amesema uwekezaji wake katika Kampuni ya Nation Media Group (NMG) unalenga kupanua shughuli za kampuni hiyo na si kupunguza wafanyakazi.
Rostam ametoa kauli hiyo leo Jumatano, Machi 11, 2026 jijini Nairobi, Kenya wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uwekezaji wake katika kampuni hiyo.
Akizungumzia mustakabali wa wafanyakazi wa kampuni hiyo, Rostam amesema hakuna mpango wa kupunguza ajira bali matarajio ni kuongeza nafasi zaidi za kazi kadri shughuli za kampuni zitakavyopanuka.
“Nataka kuwahakikishia wafanyakazi wa Nation Media Group kwamba dhamira yetu ni kupanua shughuli, si kupunguza. Kadri tunavyoendelea mbele kutakuwa na ajira zaidi kwa sababu tunahitaji kuhudumia mahitaji ya Wakenya wote,” amesema Rostam.
Nation Media Group ni moja ya kampuni kubwa za habari Afrika Mashariki ikiwa na shughuli katika nchi za Kenya, Tanzania, Uganda na Rwanda. Kampuni hiyo inachapisha magazeti mbalimbali yakiwemo Daily Nation, Sunday Nation, The EastAfrican, Daily Monitor ya Uganda pamoja na Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti nchini Tanzania. Pia inamiliki Televisheni ya NTV Kenya na Uganda na vituo vya redio Kenya, Uganda na Rwanda.
