Serikali ya Tanzania imesema kuwa licha ya mzozo unaoendelea katika eneo la Mashariki ya Kati, hadi sasa haujaonyesha athari kubwa kwa upatikanaji wa mafuta nchini, ingawa changamoto zinaweza kuibuka siku za usoni.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Petroleum Development Corporation (TPDC), Mussa Mohammed Makame, amesema kuwa hali ya sasa inatokana na uwepo wa akiba ya kutosha ya mafuta inayoweza kukidhi mahitaji ya nchi kwa miezi kadhaa ijayo.
Aidha, Mussa amesema hakuna uwezekano mkubwa wa kupanda kwa bei ya mafuta ya ndege au gharama za usafiri wa anga kwa sasa, huku serikali ikiendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa soko la kimataifa ili kuhakikisha usalama wa nishati na gharama thabiti kwa wananchi
Tanzania, kutokana na akiba yake ya kutosha, imeweza kudhibiti athari hizo kwa muda, ikihakikisha wananchi na biashara za ndani hawapati kikwazo kikubwa.
Mgogoro wa Mashariki ya Kati umekuwa chanzo cha wasiwasi wa bei za mafuta duniani, kwani nchi nyingi hutegemea usafirishaji wa mafuta kutoka eneo hilo.
