Wakala wa Nishati Vijijini imeanza utekelezaji wa mpango mkakati wa kitaifa wa nishati safi ya kupikia ili kufikia lengo la zaidi ya asilimia themanini 80% ya watanzania ifikapo mwaka 2034 wawe wanatumia nishati safi ya kupikia nishati ambayo ni salama kwa mtumiaji na rafiki kwa mazingira.
Akizungumza wakati wa ugawaji wa majiko katika Wilaya Kibondo mkoani Kigoma Mhandisi Ramadhan Mganga amesema kuwa Wakala ya Nishati Vijijini-REA mkoa huo umeanza usambazaji wa majiko banifu 8,424.
Mhandisi Mganga amesema kuwa mradi huo unahusisha usambazaji wa majiko banifu yanayotumia kuni na mkaa kidogo ili kupunguza matumizi ya vyanzo hivyo vya nishati pamoja na athari za moshi zitokanazo na matumizi katika majiko ya kawaida. Katika mkakati huo Wakala wa Nishati Vijijini umeandaa mpango wa uuzwaji wa majiko banifu 200,000 kwa bei ya ruzuku yenye ufanisi mkubwa katika utumiaji wake.
“Mikataba hii imesainiwa tarehe 09 Mei, 2025 na itatekelezwa ndani ya miezi 15. Gharama ya mradi kwa mkoa wa Kigoma ni TZS 429,539,760.00 ambapo Serikali imeroa ruzuku ya TZS 365,108,796.00,” Amesema Mha. Mganga.
Amesema mtoa huduma ni Envotec Services ambapo jumla ya majiko banifu 8,424 yatauzwa kwa wananchi kwa bei ya ruzuku. Gharama ya jiko moja ni TZS 50,990 lakini serikali imetoa ruzuku ya asilimia 85.
Akizindua rasmi majiko hayo, Mkuu wa Wilaya ya Kibondo, Aggrey Magwaza, amesema majiko hayo yaliyotolewa kwa awamu hii yataleta manufaa makubwa kwa wananchi na kusisitiza kuwa waliopata fursa ya kuyapata wayatumie kwa matumizi ya nyumbani badala ya kuyafanya biashara.
“Wilaya ya kibondo itanufaika na majiko banifu 1404 ambapo kila kaya itanufaika kwa kununua jiko moja kwa gharama ya shiringi 7,649 punguzo la asilimia 85% kutoka kwenye bei harisia ya shilingi 50,990,” Amesema DC Magwaza.
Kwa upande wao wananchi ambao wamenufaika na majiko hayo wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuamua kutoa majiko bunifu kwa bei ya ruzuku ambayo itawanufaisha wananchi wote.
