Shirika la ndege la Tanzania, Air Tanzania limetangaza mpango wa kuwarejesha nyumbani raia wa nchi hiyo walioathiriwa na hatua ya kusitishwa kwa safari za ndege kufuatia mgogoro uliozuka eneo la Mashariki ya Kati baada ya Marekani na Israel kuishambulia Iran na kumuua Kiongozi Mkuu Ayatollah Ali Khamenei Jumamosi iliyopita.
Katika taarifa iliyotolewa leo Ijumaa Machi 6, Air Tanzania imesema ndege hiyo maalum itasafiri kutoka Dar es Salam kuelekea Dubai na kurejea Dar es Salaam siku ya Jumapili.
Imesisitiza ndege hiyo sio ya kibiashara na kuongeza kwamba itawapatia kipaumbele wasafiri ambao walikuwa wamekata tiketi kabla ya safari kusitishwa.
Mashirika ya ndege ya kimataifa yalikiahirisha safari za kuelekea Mashariki ya Kati tangu Iran ilipoanza kulipiza kisasi hatua ya Marekani na Israel dhidi yake kwa kushambulia kambi za jeshi la Marekani zilizo katika mataifa ya Kiarabu katika eneo hilo.
Ndege zinazoingia na kutoka katika viwanja vya ndege vya Tel Aviv, Dubai, Doha na vituo vingine vya kimataifa katika eneo hilo zimesitishwa.
