Na Clement Shawishi – Geita
Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela amesema zoezi la kufukua mashimo manne yaliyotitia Machi 29 mwaka huu katika mgodi wa Msasa Wilayani Bukombe limekamilika bila madhara yoyote kwa binadamu.
Shigela amesema hayo wakati akipokea ripoti ya vyombo vya usalama katika mkutano uliowakutanisha wachimbaji, wamiliki wa leseni ya uchimbaji mgodi wa Msasa na wadau wengine Wilayani Bukombe Mkoani Geita.

Amesema shughuli za uchimbaji zitarejea mgodini hapo baada ya ukaguzi wa Wizara ya Madini kukamilika na kwamba Wachimbaji hawanabudi kuwa na subira na utulivu wakati ukaguzi huo ukisubiriwa kipindi hiki ambacho shughuli zimesitishwa.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Geita Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Safia Jongo amekemea vikali taarifa potofu kuhusu ajali mgodini hapo zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii na maeneo mengine na kwamba Jeshi la Polisi halitasita kuwachukulia hatua watakaohusika kutoa taarifa hizo.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoani Geita Mrakibu Msaidizi Kenneth Mwakasitu amewarai Wachimbaji kuendelea kuzingatia elimu inayotolewa kuhusu usalama mahala pa kazi zao na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano panapohitajika.
Machi 29 mwaka huu maduara manne yalititia katika mgodi wa uchimbaji dhahabu wa Msasa Wilayani Bukombe Mkoani Geita ambapo kulingana na taarifa ya Jeshi la Polisi Mkoani humo hakuna madhara kwa binadamu yaliyojitokeza.
