Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Reuben Kwagilwa, ameiagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Mamlaka ya Bonde la Wami/Ruvu na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kufanya mapitio upya ya vibali vya usafishaji wa Mto Msimbazi ili kuhakikisha havitumiki vibaya.
Kwagilwa ametoa maelekezo hayo wakati wa ziara ya kukagua hali ya mazingira katika maeneo yanayopitiwa na mto huo jijini Dar es Salaam, kufuatia malalamiko ya wananchi kuwa baadhi ya shughuli za usafishaji zimegeuka kuwa uchimbaji wa mchanga unaoharibu mazingira.
Akiwa katika daraja la Kinyerezi, kata ya Ukonga, amesema Serikali haitakubali kuona miundombinu iliyowekezwa kwa gharama kubwa ikiharibiwa kutokana na matumizi yasiyo sahihi ya vibali hivyo.
Amezitaka taasisi husika kufanya ukaguzi wa maeneo yote yenye vibali vya usafishaji wa mito ili kujiridhisha na hali halisi na kuhakikisha shughuli hizo zinalenga kulinda mazingira na kuboresha mtiririko wa maji badala ya uchimbaji wa mchanga.
