Mwanachuoni na mhubiri maarufu nchini, Sheikh Hilal Shawej ‘Kipozeo’, ametoa wito kwa waumini wa dini ya Kiislamu kutumia mwezi mtukufu wa Ramadhan kuimarisha stara na mapenzi katika ndoa zao.
Akizungumza katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam kwenye hafla ya futari iliyoandaliwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) usiku wa Machi 9, 2026, Sheikh Kipozeo amewahimiza wanandoa kutumia ruhusa ya kisheria waliyopewa ya kukutana usiku ili kuongeza uzao.
Sheikh Kipozeo, ambaye anajulikana kwa nasaha zake zinazochanganywa na ucheshi, amefafanua kuwa mwezi wa Ramadhan umegawanyika katika sehemu tatu kuu: Rehema, Msamaha, na Kunusuriwa na Moto, hivyo ni wakati wa neema kubwa kwa kila muumini.
Aidha, Sheikh Kipozeo amewasifu DAWASA kwa kazi yao kubwa akisema maji ndiyo msingi wa uhai wa kila kiumbe kama ilivyoelezwa katika vitabu vitakatifu, na bila maji hakuna ibada wala maisha.
