Na Clement Shawishi- GEITA
Serikali imesema kuwa uwekezaji unaofanywa na sekta binafsi mkoani Geita umeongeza fursa za ajira na kukuza mchango wa mkoa huo kwenye pato la taifa.
Naibu Waziri wa Wizara ya Viwanda na Biashara Bw. Dennis Londo amesema hayo leo baada ya kutembelea maonesho ya Wakandarasi, Wajenzi na Taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo yanayoendelea katika viwanja vya Dkt Samia mjini Geita.

Amesema Serikali inathamini nafasi ya sekta binafsi ambayo ni asilimia 70 kwenye pato la taifa na kwamba itaendelea kutekeleza malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ili kupiga hatua zaidi.
Katibu Tawala Wilaya ya Geita Bi Lucy Beda kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, amesema Serikali mkoani humo inaunga mkono juhudi za sekta binafsi katika uwekezaji na kutatua changamoto zilizopo.
Mwenyekiti wa maonesho hayo Bw. George John Mandia ameiomba Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), Serikali na wadau wengine kuwekeza zaidi mkoani Geita kutokana na ongezeko kubwa la watu, fursa na uwepo wa maeneo ya uwekezaji.
Mratibu wa Maonesho hayo yenye kaulimbiu ‘Matumizi ya Mitambo, Tija ya Ukandarasi na Sekta nyingine’ Mhandisi Benard Mwatta amesema kampuni 40 kutoka ndani na nje ya nchi na Wizara ya Viwanda na Biashara, wafanyabiashara, wachimbaji na wamiliki wa mitambo ya uchimbaji madini wameshiriki kikamilifu.

