Iran imesema iko kwenye mazungumzo na FIFA kuhusu uwezekano wa kucheza mechi zake za Kombe la Dunia nje ya Marekani, baada ya Donald Trump kuionya timu hiyo kukaa mbali na nchi hiyo wiki iliyopita.
Ubalozi wa Iran nchini Mexico umesema mamlaka ya soka ya nchi hiyo inataka mechi zao zifanyike Mexico badala ya Marekani.
Hata hivyo, inaaminika kuwa FIFA haiko tayari kubadilisha ratiba ya mechi huku ikiwa imesalia chini ya siku 100 kabla ya mashindano kuanza.

“Wakati Trump amesema wazi kuwa hawezi kuhakikisha usalama wa timu ya taifa ya Iran, hatutasafiri kwenda Marekani,” alinukuliwa akisema Mehdi Taj, rais wa Shirikisho la Soka la Iran.
“Kwa sasa tunafanya mazungumzo na FIFA ili mechi za Iran katika Kombe la Dunia zifanyike Mexico.”
Kutokuwepo kwa uhakika kuhusu ushiriki wa Iran kumeongezeka tangu kuzuka kwa mgogoro kati ya Marekani na Israel. Alhamisi iliyopita, Trump alizungumzia suala hilo kupitia mtandao wake wa Truth Social.
