Mhashamu Prosper Balthazar Lyimo amesimikwa rasmi kuwa Askofu wa kwanza wa Jimbo Katoliki Bariadi katika ibada iliyofanyika leo Machi 19, 2026, tukio lililohudhuriwa na waamini, viongozi wa dini na wageni mbalimbali.
Ibada hiyo imeongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Mwanza, Mhashamu Renatus Nkwande, ambaye pia ni Mkuu wa Metropolitan ya Mwanza,Tukio hilo limeashiria mwanzo wa uongozi mpya katika Jimbo hilo jipya lililoanzishwa mapema mwaka huu.
Jimbo Katoliki Bariadi liliundwa rasmi tarehe 8 Januari 2026 na Baba Mtakatifu Pope Leo XIV, likitokana na kugawanywa kwa Jimbo Katoliki Shinyanga, na sasa ni sehemu ya Jimbo Kuu Katoliki Mwanza,Makao makuu ya Jimbo hilo yako mjini Bariadi, ambapo Kanisa kuu kwa sasa ni Parokia ya Mwinjili Yohane huku ujenzi wa Kanisa kuu jipya la Mtakatifu Luka ukiendelea.
Akizungumza kufuatia uteuzi wake, Askofu Prosper Balthazar Lyimo alisema kuwa haikuwa rahisi kwake kupokea wito huo, lakini baada ya kusali na kutafakari alikubali kwa imani na matumaini ya kulitumikia Kanisa kwa moyo wote, Amewaomba waamini wa Jimbo hilo kumpokea na kushirikiana naye katika kujenga umoja na kuendeleza shughuli za kichungaji.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa sala, mshikamano na huduma yenye furaha, akieleza kuwa amani ina thamani kubwa kuliko mali za dunia.
ikumbukwe kuwa Askofu Lyimo alizaliwa Agosti 20, 1964 huko Kilema, Moshi. Alipadrishwa mwaka 1997 katika Jimbo Kuu la Arusha na kuhudumu katika nafasi mbalimbali za kichungaji na kiutawala ndani na nje ya nchi, ikiwemo masomo ya juu nchini Italia na Canada.
Mwaka 2014 aliteuliwa kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Arusha na Pope Francis, kabla ya kuteuliwa kuwa Askofu wa kwanza wa Jimbo Katoliki Bariadi mwaka 2026.
Jimbo Katoliki Bariadi lina jumla ya parokia 19, likihudumiwa na mapadre wa jimbo na watawa, pamoja na taasisi za elimu na afya zinazochangia huduma za kijamii kwa wananchi.
Kusimikwa kwake kunatajwa kuwa mwanzo wa safari mpya ya kiimani na kichungaji kwa waamini wa Jimbo Katoliki Bariadi.
