Marco Pastory- Ngara, KAGERA
Juhudi za kukabiliana na vitendo vya magendo katika maeneo ya mipakani wilayani Ngara mkoani Kagera zimepata nguvu mpya kufuatia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kukabidhi magari mawili wilayani humo.
Akizungumza wakati wa hafla ya kupokea magari hayo, Mkuu wa Wilaya ya Ngara Kanali Mathias Kahabi amesema ujio wa vitendea kazi hivyo utasaidia kudhibiti mianya ya magendo na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato ya serikali.
Amesema magari hayo yatasaidia kufikia maeneo yenye changamoto hasa mipakani ambako vitendo vya magendo vimekuwa vikifanyika mara kwa mara, na kusisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya TRA na vyombo vingine vya dola.

Kwa upande wake Meneja wa TRA mkoa wa Kagera Joseph Mtalemwa amesema wilaya ya Ngara ina vipenyo vingi vinavyotumiwa na wafanyabiashara haramu, hivyo magari hayo yatakuwa msaada mkubwa katika kufuatilia na kudhibiti usafirishaji wa bidhaa za magendo.
Ameongeza kuwa TRA itaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha ulinzi wa mapato ya serikali sambamba na kuboresha mazingira ya ukusanyaji kodi nchini.

