Mtayarishaji wa muziki Abbah, ambaye amehusika katika utayarishaji wa wimbo “Finale” uliowakutanisha wasanii Bien na Alikiba, amesema hafurahishwi na mjadala unaoendelea miongoni mwa mashabiki kuhusu kulinganisha ubora wa “verse” za wasanii hao wawili.
Abbah ameeleza kuwa si sahihi kuwashindanisha wasanii walioshirikiana kwenye wimbo mmoja, akisisitiza kuwa kila mmoja alitoa mchango wake kwa lengo la kuifanya kazi hiyo iwe bora zaidi.
Abbah amesema “Unashindanishaje watu walioimba wimbo mmoja? Shindanisha wimbo na wimbo mwingine, kwani wote hao wamefanya wimbo uwe bora,”.
Kwa mujibu wa Abbah, mchango wa kila msanii ndani ya wimbo huo umeifanya kazi hiyo kuwa na ubora wa hali ya juu na kuvutia zaidi kwa wasikilizaji.
Wimbo huo ulitoka Machi 25, 2026, na umepokelewa vizuri na mashabiki, ukifanikiwa kuvutia watazamaji zaidi ya milioni moja ndani ya saa 24 tangu kuachiwa kwake.
