Paroko wa Parokia ya Bikira Maria Kisasa, Sostenes Ndendya, ametoa wito kwa waumini na wananchi kwa ujumla kutafakari maisha yao kufuatia kifo cha aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Watu Wenye Ulemavu), William Lukuvi.
Akizungumza wakati wa ibada ya kumuaga marehemu, amesema kifo ni ukumbusho kuwa binadamu hana muda mwingi hapa duniani, hivyo kila mmoja anapaswa kutimiza wajibu wake kwa usahihi na kwa wakati.
Amesisitiza umuhimu wa kumwomba Mungu ili awajalie watu hekima ya kutambua na kuhesabu siku zao, pamoja na kutenda mema kwa kutumia vipaji na neema walizopewa kwa manufaa ya wengine.
Aidha, Paroko Ndendya amefananisha maisha ya binadamu na maua, akisema kuwa kama maua yanavyonyauka baada ya muda mfupi, ndivyo maisha ya mwanadamu yalivyo ya mpito huku akiwataka watu kutojisahau na kuishi kwa kufanya yaliyo mema kabla ya muda wao kufika mwisho.
