Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Pope Leo wa XIV, anatarajiwa kuanza ziara ya siku 10 barani Afrika Jumatatu ijayo, itakayompeleka katika mataifa manne ya Algeria, Cameroon, Angola na Equatorial Guinea.
Kwa mujibu wa Vatican, ziara hiyo ni miongoni mwa vipaumbele binafsi vya Papa Leo tangu achaguliwe mwaka 2025, ikiwa ni safari yake kubwa ya kwanza ya kimataifa mwaka 2026. Katika safari hiyo, atatembelea miji 11 tofauti na kutoa hotuba zaidi ya 25, huku akikutana na viongozi wa kisiasa na waumini wa kanisa.

Maafisa wa Vatican wanasema Papa Leo analenga kuhamasisha viongozi wa dunia kuelekeza juhudi zaidi Afrika, hasa katika kukabiliana na changamoto za migogoro, umaskini na ukosefu wa utulivu wa kisiasa.
Aidha, anatarajiwa kuhimiza mazungumzo ya kidini, hasa kati ya Wakristo na Waislamu, huku, viongozi wa kidini wanasema ujumbe mkuu wa Papa Leo katika ziara hii ni amani, mshikamano na kuishi kwa pamoja licha ya tofauti zilizopo katika jamii.
