Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Leo XIV, ameanza rasmi ziara ya siku 10 Barani Afrika, ambapo anatarajiwa kutembelea Mataifa manne ya Algeria, Cameroon, Angola na Guinea ya Ikweta, ziara hiyo inalenga kuimarisha mshikamano wa Kanisa pamoja na kuwasilisha ujumbe wa Kimataifa kuhusu umuhimu wa kulipa kipaumbele Bara la Afrika, ambalo linakadiriwa kuwa na zaidi ya asilimia 20 ya Waumini wa Kanisa Katoliki duniani.
Kwa mujibu wa Vatican, Papa Leo XIV anatarajia kutumia ziara hiyo kuhamasisha Jumuiya ya Kimataifa kuelekeza umakini zaidi katika changamoto zinazoikabili Afrika, zikiwemo umaskini, migogoro ya kijamii, mabadiliko ya tabianchi pamoja na upatikanaji wa huduma muhimu kama elimu na afya.
Hata hivyo, swali linalobaki ni iwapo ujumbe wa Papa Leo XIV utaweza kuchochea hatua za vitendo kutoka kwa Mataifa yenye ushawishi duniani, huku wengine wakiamini kuwa mafanikio ya ziara hiyo yatategemea dhamira ya kweli ya Viongozi wa Kimataifa kuchukua hatua madhubuti, badala ya kutoa ahadi zisizo na utekelezaji, ili kuleta mabadiliko chanya na endelevu Barani Afrika.
