Leicester City imeshuka daraja kwa mara ya pili mfululizo hadi League One, takribani muongo mmoja tu baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England (Premier League).
Kikosi hicho cha Gary Rowett kilihitaji matokeo yasiyotarajiwa ili kubaki katika Championship lakini kikatoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Hull City, kikiwa kimeingia kwenye mchezo huo kikiwa nyuma kwa pointi nane kutoka eneo salama huku kukiwa na mechi tatu pekee zilizobaki.
Timu ya Hull iliyokuwa ikipigania nafasi za mchujo (play-offs) ilithibitisha kushuka kwa Leicester katika Uwanja wa King Power. Leicester walikuwa nyuma kwa bao 1-0 kipindi cha kwanza kufuatia bao la Liam Millar, lakini walipata matumaini pale Jordan James alipofunga penalti dakika ya 52, na dakika mbili baadaye Luke Thomas akaongeza bao la pili.
Ushindi wa kwanza katika michezo nane ungeweza kuipa Leicester nafasi ya kupambana hadi mechi mbili za mwisho wa msimu, lakini bao la 15 la Ollie McBurnie msimu huu lilisawazisha na hawakuweza kupata bao la ushindi.
Leicester walianza msimu wakiwa miongoni mwa timu zilizokuwa zikipewa nafasi kubwa ya kupanda daraja baada ya kushuka kutoka Premier League mwaka uliopita.

Marti Cifuentes, aliyeteuliwa kuwa kocha majira ya kiangazi, alifutwa kazi Januari wakati timu ikiwa nafasi ya 14 kwenye msimamo wa Championship, pointi sita nyuma ya nafasi za play-offs.
Andy King alisimamia timu kwa muda mfupi na kushuhudia vipigo vinne kabla ya Gary Rowett kuteuliwa Februari.
Tangu hapo, Leicester walishinda mechi moja tu kati ya 11 walizocheza, na kuingia katika eneo la kushuka daraja kabla ya kupoteza kabisa matumaini ya kujinasua.
