Askofu wa Jimbo Katoliki la Rulenge Ngara, Severine Niwemugizi, ameadhimisha siku yake ya kuzaliwa huku akitafakari safari ndefu ya utume iliyojaa mafanikio, changamoto na huduma kwa Kanisa na jamii kwa ujumla.
Askofu Niwemugizi, ameendelea kuwa miongoni mwa viongozi wa Kanisa Katoliki waliotoa mchango mkubwa katika ukuaji wa Kanisa na maendeleo ya jamii nchini Tanzania kupitia utume wake wa muda mrefu uliodumu kwa miongo kadhaa.
Askofu Niwemugizi alizaliwa tarehe 3 Juni mwaka 1956 Mkoani Kagera, alipata daraja takatifu la upadre mwaka 1984 na kuanza kuhudumu katika kazi mbalimbali za kichungaji na malezi ya waamini.
Mwaka 1996 aliteuliwa na Hayati Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Rulenge kwa wakati huo na mwaka 1997 akawekwa wakfu rasmi kuanza jukumu la kuliongoza jimbo hilo.
Mbali na huduma yake ndani ya jimbo, Askofu Niwemugizi amewahi kushika nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya Kanisa Katoliki, ikiwemo kuwa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), nafasi iliyompa fursa ya kushiriki katika maamuzi na mwelekeo wa Kanisa nchini.
Katika kipindi chake cha uongozi, amejulikana kwa kusisitiza malezi ya kiroho, amani, haki za binadamu, mshikamano wa kijamii pamoja na maendeleo ya elimu na huduma za kijamii zinazotolewa na Kanisa katoliki kwawaumini wake.
Akiwa anaadhimisha siku yake ya kuzaliwa mwaka huu, waamini na wadau mbalimbali wa Kanisa wanapata nafasi ya kutafakari mchango wake katika kueneza Injili na kuwahudumia watu wa Mungu kwa zaidi ya miaka arobaini tangu alipopata daraja la upadre.
Akiwa anaadhimisha siku yake ya kuzaliwa mwaka huu, Askofu Severine Niwemugizi pia anatafakari safari ya takribani miaka 42 ya upadre na miaka 29 ya uaskofu, kipindi ambacho amekuwa akihudumu kwa uaminifu katika kueneza Injili, kuongoza waamini na kuchangia maendeleo ya Kanisa na jamii kwa ujumla.
