Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia,Prof.Daniel Mushi amesema Tanzania imeupokea kwa furaha ugeni wa Vyuo Vikuu na Maafisa kutoka Malaysia waliowasili Nchini kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kielimu na kupanua fursa za elimu ya juu kwa Watanzania.
Akizungumza Jijini Dar es salaam, Pro.Mushi amesema ugeni huo umeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wizara ya Elimu ya Malaysia pamoja na Taasisi ya Global Education Link (GEL), ukiwa na lengo la kuimarisha mahusiano kati ya Vyuo Vikuu vya Nchi hizo mbili.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia,Prof.Daniel Mushi katika picha
Kwa mujibu wa Prof.Mushi, hatua hiyo inaendana na mkakati wa Serikali wa kuifanya elimu ya Tanzania kuwa ya kimataifa na kuwaandaa Vijana kushindana katika soko la ajira la dunia.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Global Education Link (GEL), Abdulmalik Mollel amesema “Tunawaleta Watanzania karibu na Vyuo Vikuu vinavyotoa programu bora katika Afya, Uhandisi, Kilimo, Sayansi, Teknolojia, Biashara na Sanaa, pia kutakuwa na taarifa za ufadhili wa masomo pamoja na udahili wa papo kwa papo kwa Wanafunzi watakaokidhi vigezo,” alisema Mollel.
