Wakulima wadogo wapatao 180,000 katika Mkoa wa Kagera tayari wamesajiliwa kushiriki katika biashara ya kaboni, hatua inayotajwa kuwa fursa mpya ya kuongeza kipato kwa wananchi huku ikichochea juhudi za uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Mafanikio hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa KADERES, Leonard Kachebonao, wakati wa kikao cha wadau wa biashara ya kaboni kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, kikiongozwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Dk Richard Muyungi.
Kachebonao alisema kuwa licha ya kampuni hiyo kuwa changa, imefanikiwa kusajili wakulima wadogo 180,000 katika Mkoa wa Kagera, huku hatua ya usajili ikiendelea katika wilaya mbalimbali za mkoa huo kutokana na mwitikio mkubwa wa wananchi.
“KADERES imeendelea kufanya kazi kwa karibu na jamii ili kuhakikisha wananchi wanashiriki kikamilifu katika miradi ya kaboni. Hadi sasa tumefanikiwa kusajili wakulima 180,000 na bado tunaendelea na zoezi hilo katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Kagera,” alisema Kachebonao.
Alifafanua kuwa shughuli za kampuni hiyo zinafanyika katika karibu wilaya zote za Mkoa wa Kagera isipokuwa Manispaa ya Bukoba, huku maandalizi ya kuanza utekelezaji wa shughuli hizo yakikamilishwa.
Akizungumza katika kikao hicho, Dk Muyungi alisema maendeleo na ukuaji wa biashara ya kaboni nchini yanapaswa kwenda sambamba na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, akisisitiza kuwa sekta hiyo ni miongoni mwa nyenzo muhimu zitakazochochea ukuaji wa uchumi, uhifadhi wa mazingira na ustawi wa wananchi katika kipindi cha miongo ijayo
