Mahujaji wa Kitanzania wameanza kurejea nchini baada ya kukamilisha ibada ya Hija katika Miji Mitakatifu ya Makkah na Madina nchini Saudi Arabia, huku wakieleza kuwa amani na utulivu uliopo Tanzania umechangia kuwawezesha kutekeleza ibada hiyo muhimu ya Kiislamu.
Akizungumza mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam, Hujaji Said Njuki amesema anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwawezesha kwenda na kurejea salama kutoka katika ibada hiyo ambayo ni Nguzo ya Tano ya Uislamu.
Njuki amesema hali ya amani na utulivu iliyopo nchini imeendelea kuwa chachu kwa waumini wa dini ya Kiislamu kutekeleza majukumu yao ya kidini kwa uhuru na utulivu, akibainisha kuwa mazingira ya migogoro au vita yangeweza kuwa kikwazo kwa utekelezaji wa ibada hiyo.
Aidha, amezishukuru taasisi zinazoratibu safari za Hija kwa mchango wake katika kuhakikisha mahujaji wanapata huduma stahiki na kutekeleza ibada zao kwa usalama, akitaja miongoni mwa taasisi hizo Taasisi ya Manasik Hajji and Umrah.
Kwa upande wao, Ramadhani Issa Hassani na Athumani Lusewa kutoka Taasisi ya Manasik Hajji and Umrah wamewahimiza Waislamu wenye uwezo wa kimwili na kifedha kujiandaa kutekeleza ibada ya Hija, wakieleza kuwa ni wajibu muhimu kwa kila Muislamu mwenye uwezo.
Wamesema mafanikio ya mahujaji wa Tanzania katika msimu huu wa Hija yanaakisi umuhimu wa kuendeleza ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Saudi Arabia pamoja na kuimarisha huduma za uratibu wa safari hizo ili waumini waweze kutekeleza ibada zao katika mazingira salama na yenye utaratibu.
