Papa Leo wa XIV amekutana na Waziri Mkuu wa Hispania, Pedro Sánchez Pérez-Castejón, katika mkutano mfupi wa faragha uliofanyika jijini Madrid asubuhi ya Jumatatu, Juni 8, 2026.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Habari ya Kiti Kitakatifu, mkutano huo wa takribani dakika 20 ulifanyika kabla ya Papa kuelekea katika Bunge la Manaibu la Hispania kwa ajili ya kukutana na wabunge, ikiwa ni sehemu ya ratiba ya siku ya tatu ya Ziara yake ya Kitume nchini humo.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa baada ya mazungumzo hayo ya faragha, Papa Leo XIV alipata fursa ya kuwasalimia baadhi ya washirika wake kabla ya kuendelea na shughuli nyingine zilizopangwa katika ziara hiyo.
Huu ni mkutano wa pili kati ya viongozi hao katika kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja, baada ya kukutana kwa mara ya mwisho mjini Vatican mnamo Mei 27, 2025.
Ziara ya Papa Leo XIV nchini Hispania inaendelea huku ikijumuisha ratiba mbalimbali za kichungaji, kidiplomasia na kijamii zinazolenga kuimarisha mahusiano kati ya Kanisa Katoliki na jamii ya Hispania.
