Mbunge wa Jimbo la Kawe, Timoth Geofrey Anyosisye, amesema lugha ya Kiswahili ni fursa muhimu kwa Tanzania kutokana na kuendelea kuenea na kutumiwa kwa kiwango kikubwa nchini na katika mataifa mbalimbali ya Afrika Mashariki.
Akizungumzia umuhimu wa ushiriki wa Tanzania katika Kongamano la Pili la Kimataifa la Kiswahili nchini Ufaransa, Anyosisye amesema kongamano hilo linafungua milango ya kuitangaza na kuieneza lugha ya Kiswahili katika mataifa mengi duniani.
Amesema Kiswahili ni sehemu ya utambulisho wa taifa na urithi wa kitamaduni unaopaswa kuendelezwa na kutangazwa kimataifa ili kuongeza mchango wake katika mawasiliano, elimu, biashara na diplomasia.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika ukuzaji wa Kiswahili ili kiweze kunufaisha Watanzania kiuchumi na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika jukwaa la kimataifa.
