Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) imewataka wanawake kutumia teknolojia ya Akili Unde kwa hekima na maadili ili kulinda utu wa binadamu na kuimarisha amani katika familia na jamii.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa WAWATA Taifa anayemaliza muda wake, Evaline Malisa Ntenga, wakati wa Mkutano Mkuu wa 47 wa WAWATA unaofanyika katika Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) huko Jimbo Katoliki la Singida kuanzia Juni 4 hadi 7, 2026.
Akizungumza katika mkutano huo uliofunguliwa kwa Misa Takatifu iliyoongozwa na Askofu Edward Elias Mapunda, Ntenga amesema maendeleo ya teknolojia yanapaswa kwenda sambamba na maadili, utu na heshima kwa binadamu.
Amesema matumizi mabaya ya Akili Unde yanaweza kusababisha migawanyiko, upotoshaji wa taarifa na kudhoofisha mahusiano ya kijamii, huku akitolea mfano matumizi ya teknolojia hiyo kutengeneza picha za uongo na taarifa zisizo sahihi zinazoweza kuwapotosha watu.
Ntenga amerejea mafundisho yaliyomo katika waraka wa kitume wa Papa Leo XIV, Magnifica Humanitas, unaosisitiza kuwa teknolojia inapaswa kuwa chombo cha kuhudumia binadamu na si kutawala maisha yake.
Aidha, amesema wanawake wana jukumu la msingi katika malezi ya familia na wanapaswa kuhakikisha watoto wanalelewa katika mazingira yanayowajengea maadili mema na matumizi sahihi ya teknolojia.
Mkutano huo wa WAWATA pia umetumika kutathmini mafanikio ya jumuiya hiyo, kujadili mustakabali wa wanawake Wakatoliki nchini na kujiandaa kwa uchaguzi wa viongozi wapya, huku wajumbe wakihimizwa kuzingatia umoja, uwajibikaji na ustawi wa Kanisa na jamii kwa ujumla.
