Wakristo wamehimizwa kuendelea kumsikiliza Mungu, kutokata tamaa wanapokutana na changamoto mbalimbali za maisha na kuendelea kuishuhudia Injili kwa ujasiri licha ya vikwazo na mateso wanavyoweza kukumbana navyo.
Wito huo umetolewa na Paroko Msaidizi wa Parokia ya Ngara Mjini Jimbo Katoliki la Rulenge-Ngara wakati akitoa homilia takatifu kupitia kipindi cha Tumwimbie Bwana kinachorushwa na Radio Kwizera FM.
Katika mahubiri yake, amesema kuwa safari ya imani si rahisi kwani mara nyingi waumini hupitia nyakati ngumu zinazoweza kuwafanya waone kana kwamba hakuna matumaini au mwanga mbele yao, huku akiwakumbusha kuwa Yesu Kristo anawataka waamini kuendelea kuwa na moyo wa matumaini na kutokata tamaa hata wanapokabiliwa na magumu.
Aidha, amesisitiza kuwa jukumu la kueneza Injili si la maaskofu, mapadre, watawa na makatekista pekee, bali ni wajibu wa kila Mkristo aliyebatizwa na kwamba kila muumini anaitwa kumshuhudia Kristo kwa maneno na matendo, kwa kuikiri, kuiishi na kuiungama imani yake mbele ya watu wote.
Katika hatua nyinghine Padre Ademba amewataka waumini kusimama upande wa ukweli bila hofu, akieleza kuwa mara nyingi ukweli huweza kuumiza lakini ni msingi muhimu wa maisha ya Kikristo. Huku akiwasihii waumini kujiepusha na vitendo vinavyomtenga mwanadamu na Mungu, ikiwemo kutafuta msaada kwa waganga wa kienyeji na kuabudu miungu mingine, badala ya kumtegemea Mungu katika changamoto zao.
Amewataka kaumini kuendelea kuwa mashuhuda wa kweli wa Injili katika familia, sehemu za kazi na jamii kwa ujumla, wakiamini kuwa Mungu huwa pamoja nao katika kila hatua ya maisha yao.
