Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) umetangaza fursa za uwekezaji katika miradi sita mikubwa ya kimkakati ya barabara kupitia mfumo wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), hatua inayolenga kuharakisha maendeleo ya miundombinu nchini huku ikipunguza utegemezi wa fedha za Serikali.
Hatua hiyo pia ni sehemu ya mageuzi ya kisheria na kisera yanayotekelezwa na Serikali ya Tanzania ili kuvutia mitaji kutoka sekta binafsi kwa ajili ya kugharamia miradi mikubwa ya maendeleo, ikiwa na lengo la kuongeza kasi ya ujenzi wa miundombinu ya uchumi.
Miradi hiyo itatekelezwa kwa mfumo wa kubuni, kujenga, kugharamia, kuendesha, kutunza na baadaye kuikabidhi Serikali, maarufu kama Design, Build, Finance, Operate and Transfer (DBFOT).
Mkurugenzi Mtendaji wa PPP Centre, David Kafulila amepongeza hatua ya Tanroads kutangaza fursa hizo kwa uwazi ndani na nje ya nchi, akisema itawawezesha wawekezaji wakubwa kushiriki kwa ushindani wa haki na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa miradi.
Kafulila amesema hatua hiyo pia itawapa Watanzania nafasi ya kufuatilia kwa karibu maendeleo ya miradi hiyo muhimu ya barabara, ambayo inatarajiwa kuboresha usafiri na kuchochea ukuaji wa uchumi katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Miradi iliyotangazwa ni pamoja na upanuzi wa barabara ya Morogoro–Dodoma (km 260), Chalinze–Segera–Tanga (km 246), Handeni–Kiberashi–Chemba–Kwamtoro–Singida (km 384), mteremko wa Mlima Kitonga (km 27), Expressway ya Dar es Salaam–Kibaha (km 42) na Expressway ya katikati ya Jiji la Dar es Salaam hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) yenye urefu wa kilometa 10.
