Na Clement Shawishi – Geita
Serikali Mkoani Geita imeahidi kuendelea kuthamini na kuhamasisha matumizi ya teknolojia katika sekta ya madini ili kuongeza tija katika uzalishaji na ushiriki wa Watanzania wengi kwenye sekta hiyo muhimu.
Mkuu wa Wilaya ya Geita Bw. Hashim Komba amesema hayo mjini Geita wakati akizindua Mtambo wa kisasa mahususi kwa kutengeneza na kusambaza vilipuzi kwaajiri ya shughuli za uchimbaji madini.

Amesema Mtambo huo unaojulikana kama Mobile Manufacturing Unit (MMU) wenye thamani ya zaidi ya shilingi Milioni 600 utasaidia kupunguza ajali na kuongeza usalama wa Wafanyakazi Migodini.Kaimu Ofisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Geita Mhandisi Gasper Kachenge amesema Ofisi yake imejipanga kusimamia vyema Kampuni zote za uchimbaji madini kwa kuzingatia Sheria na Viwango vinavyotakiwa.
Kwa upande wake kaimu Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Geita Mrakibu Msaidizi Kenneth Mwakasitu amesema elimu ya usalama mahala pa kazi hususani migodini ni muhimu kutolewa licha ya matumizi ya teknolojia kuongezeka na kwamba itasaidia kupunguza ajali.

Uzinduzi wa Mtambo huo unatajwa kuwa hatua muhimu katika kuimarisha matumizi ya teknolojia ya kisasa migodini na ongezeko la ushiriki wa wawekezaji wazawa kwenye sekta zinazochangia asilimia kubwa ya pato la Taifa.
