Na Michael Mpunije- Kasulu, Kigoma
Zaidi ya Vibanda 50 vya wafanyabiashara katika soko la kijiji cha Mvinza kata ya Kagerankanda Halmshauri ya Wilaya ya Kasulu Mkoani kigoma vimeteketea moto kutokana na hitilafu ya Umeme na kusababisha hasara kwa Wafanyabiashara.
Akizungumza kwa njia ya simu mwenyekiti wa kijiji cha Mvinza Bw. Denis Kavula amesema moto huo ulizuka majira ya saa tano usiku wa kuamkia leo June 23 ambapo jitihada za kuzima moto huo zilishindikana licha ya wananchi kufanikiwa kuokoa baadhi ya mali za wafanya biashara hao.

Amesema chanzo cha Moto huo unadhaniwa kuwa ni hitilafu ya umeme iliyotokea katika vibanda viwili vya soko hilo huku akieleza kuwa athari imekuwa kubwa kutokana na bidhaa za wafanyabiashara kuteketea kwa moto.
Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Mvinza kata ya Kagerankanda wameliomba Jeshi la zima moto na Uokoji wilaya ya Kasulu kuendelea kutoa elimu ya namna ya kukabiliana na majanga ya Moto ili kuendelea kuchukua tahadhari pindi majanga hayo yanapotokea.

