Na Naomi Milton- KIGOMA.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro, amewataka wananchi kuzingatia ubora na uimara wa nyumba wanazojenga ili kupunguza athari zinazoweza kusababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha.
Wito huo umetolewa wakati wa kukabidhi msaada kwa kaya 121 katika Manispaa ya Kigoma Ujiji zilizoathirika na maafa yaliyosababishwa na mvua hizo.

Balozi Sirro amesema wananchi wanapaswa kuchukua tahadhari katika kipindi hiki cha mvua kwa kuhakikisha makazi yao yanajengwa kwa kuzingatia viwango vinavyoweza kuhimili changamoto za hali ya hewa.
Amesisitiza kuwa hatua za kujikinga na majanga zinapaswa kuanza kabla ya maafa kutokea, badala ya kusubiri madhara yatokee na kusababisha uharibifu wa mali na makazi.
Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Hashim Mvogogo, jumla ya nyumba 121 zimeathirika katika Kata za Gungu, Kibirizi, Mwanga Kusini na Katubuka, huku Halmashauri ikitoa tani 2.6 za mchele, tani 1.9 za unga wa mahindi, tani moja ya maharage na mahitaji mengine kwa waathirika.
