
Na Enock Yoronimo- Bukoba, Kagera
KAGERA: Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali Yahya Kido, amesema jumla ya kaya 38,217 zenye wakazi 84,934 zinatarajiwa kunufaika na awamu ya pili ya mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, unaolenga kuongeza wigo wa wananchi wanaopata huduma za matibabu mkoani humo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa awamu ya pili katika Manispaa ya Bukoba kimkoa Kanali Kido amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira yatakayowawezesha wananchi kupata matibabu bila kukabiliwa na changamoto kubwa za gharama, hususan wale wanaoishi katika mazingira magumu kiuchumi.
Kido amesema kaya nyingine, vikundi na vyama vya ushirika vitachangia Tsh 150,000/- kwa mwaka, huku kifurushi husika kikitarajiwa kuwezesha watu sita kupata huduma za matibabu
Amesema kaya maskini zinazotambuliwa rasmi zitasajiliwa na Serikali bila kulazimika kuchangia fedha, hatua inayolenga kuhakikisha wananchi wenye kipato cha chini wanapata huduma za afya wanapozihitaji.
Aidha baadhi ya Wananchi katika Manispaa ya Bukoba wamesema kutolewa Kwa Bima hizo itasaidia kupunguza usumbufu uliokuwa unajitokeza wakati wa kupata huduma za matibabu.
