MKURUGENZI Mkazi wa AGRA Tanzania, Vianey Rweyendela amesema uwekezaji mkubwa katika sekta ya kilimo ni muhimu ili kuchochea ukuaji wa uchumi na kuboresha maisha ya wananchi kwa kuwa ndiyo sekta inayoajiri watu wengi nchini.
Rweyendela alisema hayo leo jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu matokeo ya ziara ya kutembelea miradi inayotekelezwa kwa ushirikiano kati ya AGRA, Serikali na wadau wa maendeleo katika mikoa ya Kigoma, Rukwa, Katavi, Tabora na Dodoma.
Amesema ili wananchi wanufaike na ukuaji wa uchumi, ni lazima nguvu kubwa ielekezwe katika sekta ya kilimo kwa kuwa ndiyo inayobeba ajira kwa idadi kubwa ya Watanzania.
Alisema kuwepo kwa maeneo mengi ya biashara na huduma katika mkoa huo ni ushahidi wa mabadiliko makubwa ya kiuchumi yanayotokana na uwekezaji katika kilimo na miundombinu.
Rweyendela amesema alifika Majimoto kwa mara ya kwanza mwaka 2017 wakati AGRA ilipoanza kutekeleza Mkakati wake wa Pili (AGRA 2.0), ambapo eneo hilo lilikuwa linakabiliwa na mafuriko na halikuwa na maendeleo makubwa.
Amesema kwa sasa Majimoto imebadilika na kuwa kitovu cha biashara chenye viwanda, benki, hoteli na huduma nyingine muhimu, hali inayodhihirisha mafanikio ya uwekezaji uliofanyika.
Aliongeza kuwa mabadiliko hayo yanaonyesha kuwa uwekezaji katika kilimo una uwezo wa kuchochea maendeleo ya maeneo ya vijijini na kuyageuza kuwa vituo muhimu vya shughuli za kiuchumi.
