Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (FCID) imefungua mashtaka dhidi ya mwanzilishi wa Aristokrat Records Piriye Isokrari ambayo imemlea mwanamziki Burna Boy kutoka nchini Nigeria, ikimtuhumu kwa ubadhirifu, udanganyifu wa kifedha na kukiuka wajibu wa kisheria.
Mashitaka haya yanakuja baada ya kuzuka mgogoro mkubwa wa kisheria kuhusu umiliki wa kazi za awali za muziki za Burna Boy, ukizikutanisha kampuni yake ya sasa ya Spaceship Music na lebo iliyomlea awali, Aristokrat Music, pamoja na mshirika wake wa kibiashara, 960 Music Group.
Chanzo cha mgogoro huo ni mauzo yanayodaiwa kufanyika Mei/Juni 2024, ambapo Aristokrat Music inadaiwa kuuza haki miliki (IP) na master recordings za awali za Burna Boy kwa Spaceship Music, kampuni inayomilikiwa na msanii huyo na mama yake, Bose Ogulu.
Hata hivyo, 960 Music Group, ambayo inamiliki asilimia 40 ya Aristokrat Music, imepinga vikali mauzo hayo ikidai yalifanyika kinyume cha sheria bila ridhaa ya wanahisa wala idhini ya bodi.
Kutokana na hilo, 960 Music imefungua kesi katika Mahakama Kuu ya Shirikisho huko Port Harcourt, ikitaka mauzo hayo yatangazwe kuwa batili. Kampuni hiyo inasisitiza kuwa mali hizo zilikuwa rasilimali kuu za kampuni na haziwezi kuuzwa bila makubaliano ya pamoja.
Zaidi ya mgogoro wa madai ya kiraia, sakata hilo sasa limeingia kwenye mkondo wa jinai ambapo lebo hiyo inadaiwa kuelekeza mapato ya mauzo hayo kwa matumizi binafsi au nje ya akaunti rasmi za kampuni.
Kwa upande wa Burna Boy, mgogoro huu unaweka hatarini udhibiti wa kazi zake za awali kama Like to Party na Tonight.
Endapo mahakama itaamua kwa upande wa 960 Music, Spaceship Music huenda ikalazimika kurejesha haki hizo kwa wamiliki wa awali, na hivyo kuziacha kazi hizo katika sintofahamu ya kisheria.
