Msanii mkongwe wa Bongo Fleva na aliyewahi kuwa member wa TMK Wanaume Family, Amani Temba, amesema aliwahi kuondolewa kwenye mafunzo ya JKT kutokana na tattoo alizokuwa nazo mwilini pamoja na masuala ya muziki. Temba anasema tattoo hizo zilikuja kuonekana wakati wa mapumziko, baada ya kwenda kuogelea na wenzake.
Baada ya kuondoka JKT, Temba aliamua kuendelea na elimu ambapo alijiunga na Chuo cha Bandari jijini Dar es Salaam, ambako alisomea ukaguzi wa mizigo na bidhaa bandarini hadi ngazi ya shahada.
Katika maisha yake binafsi, Temba alifunga ndoa mwaka 2008 katika eneo la Azania Front jijini Dar es Salaam. Kwa taarifa zilizopo, alibarikiwa kupata watoto wanne, ingawa haijafahamika kama familia yake imeongezeka.
Temba ambaye amekuwa msiri kuhusu maisha yake binafsi, bado ana historia ndefu ndani na nje ya muziki. Safari yake kutoka TMK Wanaume Family, JKT, elimu hadi maisha ya familia inaendelea kuwa sehemu ya stori yake.
