Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limetumia Mkutano wa 12 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Nairobi (COP12) unaofanyika Dar es Salaam, kuimarisha ushirikiano katika uhifadhi wa mazingira ya bahari na pwani pamoja na kukuza Uchumi wa Buluu endelevu.
Mkutano huo unaofanyika kuanzia tarehe 6 hadi 9 Oktoba 2026 katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC), umeenda sambamba na maadhimisho ya miaka 40 ya Mkataba wa Nairobi na umebeba kaulimbiu: “Towards Sustainable Blue Economy in the Western Indian Ocean Region for People and Nature: A Journey of Forty Years.”
Kupitia mkutano huo, NEMC inashiriki katika majadiliano ya kikanda yanayolenga kushughulikia changamoto za uchafuzi wa bahari, mabadiliko ya tabianchi, uhifadhi wa bioanuai na matumizi endelevu ya rasilimali za bahari na pwani.
Aidha, jukwaa hilo linatoa fursa kwa NEMC kuimarisha ushirikiano na taasisi za kitaifa, kikanda na kimataifa katika kubadilishana uzoefu, utaalamu na teknolojia za usimamizi wa mazingira.
NEMC pia inalenga kutumia fursa zinazopatikana kupitia COP12 katika kuimarisha ushirikiano wa kifedha na kitaalamu kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya mazingira, ikiwemo uhifadhi wa bioanuai, tafiti, udhibiti wa uchafuzi na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Ushiriki huo unaendelea kuiwezesha Tanzania kuwasilisha masuala yake ya kimazingira katika ngazi ya kikanda, huku ukifungua fursa za ushirikiano na rasilimali zitakazosaidia kuimarisha uhifadhi wa mazingira ya bahari na pwani na maendeleo ya Uchumi wa Buluu.
