Sekta ya utalii, biashara, kilimo na viwanda imeendelea kuwa miongoni mwa vichocheo muhimu vya shughuli za kiuchumi mkoani Arusha, huku matumizi ya mifumo ya kidijitali yakitajwa kuwa muhimu katika kurahisisha malipo na ukusanyaji wa mapato.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI), Dkt. Ernest Mjingo, amesema mifumo ya kisasa ya kifedha imekuwa na mchango katika kurahisisha miamala inayohusiana na shughuli za utalii na biashara, ikiwemo ukusanyaji wa mapato.
Dkt. Mjingo ameyasema hayo jijini Arusha wakati wa kikao cha wadau wa biashara na wateja wakubwa wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), kilicholenga kujadili fursa na mahitaji ya sekta mbalimbali zinazochangia uchumi wa mkoa huo.
Amesema Arusha inaendelea kushuhudia ongezeko la shughuli za utalii pamoja na ukuaji wa biashara, kilimo na viwanda, hali inayohitaji mifumo madhubuti ya kifedha na kidigitali ili kurahisisha shughuli za kiuchumi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Wateja Wakubwa na Serikali wa NBC, Elvis Ndunguru, amesema ukuaji wa utalii unahitaji huduma za kifedha zinazoendana na mahitaji ya wafanyabiashara na wawekezaji, hasa katika maeneo ya malipo na ukusanyaji wa mapato.
Amesema benki hiyo imeendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali katika matumizi ya mifumo ya kidigitali ya malipo, ikiwemo GePG na MUSE, pamoja na mifumo inayohusisha taasisi za uhifadhi kama TANAPA na NCAA.
