KIUNGO wa Manchester United na timu ya taifa ya Ureno, Bruno Fernandes amesema Cristiano Ronaldo bado ni alama kubwa zaidi ya soka nchini hiyo licha ya kuondoka kambini baada ya kufahamishwa kwamba hatakuwa kwenye kikosi cha kwanza.
Ronaldo (41), aliondoka kambini baada ya Kocha Jorge Jesus kumwambia hatakuwa katika kikosi cha kwanza dhidi ya Denmark kwenye Ligi ya Mataifa, mchezo ambao Ureno ilishinda mabao 4-2 bila uwepo wa nahodha huyo.
Nyota huyo wa zamani wa Real Madrid na Manchester United ndiye kinara wa mabao na mechi kwa Ureno, akiwa amefunga mabao 146 katika mechi 234. Pia aliisaidia nchi yake kutwaa Euro 2016 na Ligi ya Mataifa mara mbili.Hata hivyo, kuondoka kwake kambini kumeibua maswali kuhusu hatma yake katika kikosi hicho.

Ureno ilitwaa Ligi ya Mataifa mwaka 2019 na ni mabingwa watetezi baada ya kuifunga Hispania kwa penalti katika fainali ya mwaka 2025, kufuatia sare ya mabao 2-2 ndani ya dakika 120, huku Ronaldo akifunga bao moja.
Katika michuano hiyo, Ureno ilianza kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Wales, huku Ronaldo akicheza dakika 67, kabla ya kuwa benchi bila kutumika katika ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Norway.
