Pengo la mitaji kwa uzalishaji, uhifadhi na usafirishaji wa korosho limefungua fursa ya kupanua huduma za kifedha kwa wakulima na vyama vya ushirika kusini mwa Tanzania. Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imepanua mikopo na bima kuwawezesha wakulima kuongeza uzalishaji.
Hatua hiyo imekuja wakati NBC ikizindua msimu wa tano wa kampeni ya “Wekeza NBC Shambani Ushinde, Tunakuona Mbali Mkulima” katika Mtwara, Lindi na Ruvuma. Kampeni hiyo inatoa mikopo ya pembejeo, matrekta, malori na maghala, pamoja na bima ya mazao na afya.
Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba, Kanali Mstaafu Michael Mtenjele, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, amewataka wakulima kuweka akiba, kutumia bima na kupanga matumizi ya fedha ili kuongeza uwekezaji katika kilimo.
Mkurugenzi wa Wateja Wadogo wa NBC, Elibariki Masuke, amesema benki hiyo inasogeza huduma karibu na wakulima kupitia njia za kidigitali na mawakala, kuwawezesha kupata mikopo na bima bila kusafiri umbali mrefu.
Kampeni hiyo pia inawapa wakulima nafasi ya kushinda baiskeli na pikipiki. AMCOS zinashindania mashine za kufungia mifuko, huku Vyama Vikuu vya Ushirika vikishindania magari mawili aina ya double cabin.
