Vanessa Mdee amejivunia mafanikio ya mwenzi wake, Rotimi, ambaye ameigiza na kushiriki kama mtayarishaji mkuu wa filamu mpya ya God With Us.
Kupitia video aliyochapisha Instagram akiwa na Rotimi kwenye zulia jekundu, Vanessa amesema nyuma ya mafanikio makubwa kuna safari ya imani, kujitoa na uvumilivu, akieleza kuwa ameshuhudia juhudi alizoweka mwenzi wake katika kutengeneza filamu hiyo.
Katika chapisho jingine, Vanessa aliandika kuwa anajivunia kuwa mke wa muigizaji mkuu wa filamu hiyo na kufurahia kushuhudia mambo ambayo Mungu anaendelea kuyafanya katika maisha yake.
Kwa upande wake, Rotimi amesema filamu hiyo inalenga kuwakumbusha watu kuwa Mungu yupo pamoja nao hata wanapokumbwa na mashaka, kukosa kujiamini au kupoteza matumaini.
Ameongeza kuwa filamu hiyo inawasilisha ujumbe wa kiimani kupitia simulizi ya mapenzi na wahusika ambao watazamaji wanaweza kujitambulisha nao, bila kuwafanya wahisi kama wanahubiriwa.
Filamu hii inatarajiwa kuanza kuonyeshwa kwenye kumbi za sinema Novemba 13, 2026.
