
Na Shafiru Yusuph- Muleba, Kagera
Wadau wa maendeleo Wilayani Muleba, Mkoani Kagera, wametakiwa kushirikiana na Serikali katika kuwawezesha watu wenye ulemavu kupata fursa mbalimbali za kiuchumi zitakazowasaidia kujikwamua kimaisha.
Wito huo umetolewa na Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Muleba, Bi. Faraja Mbilinyi, wakati akizungumza na makundi ya watu wenye ulemavu, vijana na wanawake wanaojihusisha na shughuli za kilimo na ufugaji.
Amesisitiza umuhimu wa wadau kushirikiana na Serikali katika kutoa fursa na kuwawezesha makundi hayo kiuchumi ili yaweze kutumia uwezo wao kujiletea maendeleo na kuchangia maendeleo kwenye jamii.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Muleba Disability Relief and Empowerment Bw. Peradius Mgogoro amesema lengo la kukutana na makundi hayo ni kuwahamasisha kuanzisha shughuli za kilimo na ufugaji ili kuondoa hali ya utegemezi.
