Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda ameipongeza Halmashauri ya Jiji la Mwanza kwa juhudi zake za kupunguza upungufu wa madawati katika shule za elimu ya awali na msingi, akisema hatua hiyo ni kielelezo cha uwajibikaji na dhamira ya dhati ya kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.
RC Mtanda ameyasema hayo alipokuwa akikabidhi jumla ya madawati 2,939 kwa shule 13 za elimu ya awali na msingi zilizopo ndani ya Jiji la Mwanza.
Madawati hayo yametengenezwa kwa thamani ya Shilingi milioni 440,800,000 katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi huo.
Amesema kwa sasa Mkoa wa Mwanza una upungufu wa madawati elfu 61,808, huku Jiji la Mwanza likiwa miongoni mwa halmashauri zenye uhaba mkubwa zaidi.

Hata hivyo, amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji hilo kwa kuanza mchakato madhubuti wa kumaliza changamoto hiyo.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa, utekelezaji wa mradi huo utaondoa upungufu wa karibu madawati 4,000 na kubakiza takribani 2,000 pekee, ambayo ameahidi yataondolewa mapema mwaka huu.
“Nimefurahi kusikia kuwa Mkurugenzi ameahidi kumaliza kabisa uhaba wa madawati katika halmashauri yake.
Nawataka Wakurugenzi wengine waige mfano huu,” amesisitiza.
Aidha, RC Mtanda aliziagiza halmashauri zote zenye upungufu mkubwa wa madawati ikiwemo Jiji la Mwanza, Kwimba, Magu na Sengerema kuanzisha karakana za utengenezaji wa madawati ili kupunguza gharama na kuongeza kasi ya uzalishaji.

Alionya kuwa ndani ya miezi mitatu Ofisi yake itaanza kufanya ziara za ukaguzi kufuatilia uzalishaji huo, akisisitiza kuwa ifikapo mwisho wa mwaka huu changamoto ya madawati iwe historia.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Wakili Kiomoni Kibamba, amesema wamejipanga kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayekaa chini darasani. Ameeleza kuwa kipaumbele kimetolewa kwa shule zenye mahitaji makubwa na kwamba ifikapo mwezi Juni mwaka huu, madarasa yote yaliyopo yatakuwa na wastani wa madawati 30 kila moja.
